Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, kufuatia kufukuzwa, kuteswa na kufungwa gerezani kwa Mashia na baadhi ya nchi za Kiarabu, Jumuiya ya walimu wa hawza ya Qum, imetoa taarifa rasmi kujibu suala hilo.
Matini ya taarifa hiyo ni kama ifuatavyo:
بسم الله الرحمن الرحیم
Baada ya uvamizi wa kihalifu wa Marekani na Mazayuni dhidi ya Iran na ushirikiano wa baadhi ya serikali za Kiarabu za kandokando ya Ghuba ya Uajemi na tawala hizi ovu na za kishetani, mshikamano wa kipekee umejitokeza duniani kati ya taifa la Iran na mataifa ya Kiislamu kote katika ulimwengu wa Kiislamu pamoja na watu huru duniani, kuanzia mashariki hadi magharibi mwa ulimwengu wa Kiislamu, kutoka mwisho wa bara la Asia hadi ndani kabisa ya Afrika, mataifa yako pamoja na wananchi wa Iran na yanaunga mkono jibu la Iran dhidi ya wavamizi.
Katika hali hii, serikali zinazotii ubeberu hususan serikali za Kiarabu za eneo hili, kwa kutekeleza mipango ya maelekezo ya ubeberu, zinajaribu kuanzisha vita vya kimadhehebu na vita baina ya Shia na Sunni, na kwa kuweka mashinikizo dhidi ya raia wa Kishia katika nchi zao, zinawafanyia vitendo vya kidhalimu na vya kinyama. Kufukuzwa, mateso na vifungo ni sehemu ya tabia hizi za kupinga ubinadamu, na bila shaka mwelekeo wa vitendo hivi umetokana na njama za Kizayuni na Kimarekani.
Chanzo cha misingi ya kisiasa ya Iran ni: «اَشِدّاءُ عَلَی الکُفّارِ رُحَماءُ بَینَهُم» na katika uhusiano huu inasisitiza misingi yake ya Kiislamu. Umma wa Kiislamu unatakiwa kufahamu kuwa popote ambapo uadui na chuki zimeenezwa kati ya jamii za Kiislamu, mkono wa shetani umekuwa ukihusika: «اِنَّما یُریدُ الشَّیطانُ اَن یُوقِعَ بَینَکُمُ العَداوَةَ وَالبَغضاء».
Jumuiya ya walimu wa hawza ya Qum, inalaani kwa nguvu zote vitendo vya kupinga Uislamu na vya kinyama dhidi ya jamii ya Mashia na wanazuoni wa dini katika nchi za Bahrain, Kuwait, Imarati na nchi nyingine za Kiarabu, na huku ikionesha masikitiko makubwa juu ya watawala hawa kuwa mbali kiasi hiki na mafundisho ya Qur’ani, inasisitiza kwamba; uwezo wote wa ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuelekezwa katika kusimamisha ubeberu na utawala vamizi wa Kizayuni, kisha kuusukuma nyuma ulimwengu wa ubeberu na kuondoa utawala wao katika eneo hili, na jambo hili ni wajibu wa kiimani.
Uwepo wenye nguvu wa fikra za Kishia katika maeneo nyeti ya Mashariki ya Kati kama Iran, Iraq na Lebanon unahesabiwa kuwa tishio kubwa kwa maslahi ya Marekani na Israel, na fikra hii inafuatilia umoja wa Kiislamu dhidi ya maadui. Kwa hiyo, hatua yoyote dhidi ya Mashia ni hatua ya Kimarekani na Kizayuni, na serikali za Kiarabu kupitia vitendo vyao dhidi ya Mashia zinafanya mwenendo wa kimamluki.
Tunawaomba wanazuoni wa ulimwengu wa Kiislamu wasimame kwa uthabiti dhidi ya ubeberu na wabatilisha njia ya kueneza mifarakano na kuanzisha migogoro kati ya Sunni na Shia. Iran ya Kiislamu ni rafiki wa majirani zake na Umma wote wa Kiislamu, na harakati hizi za kupinga Mashia hazitowapatia njia yoyote ya kutoka katika mgogoro.
Tunatumaini kwamba Umma wa Kiislamu na wanazuoni wa ulimwengu wa Kiislamu watatumia uwezo wote wa kifikra na kiutendaji katika kuzima njama za kupinga Uislamu, na kwa umoja dhidi ya ubeberu wawe nguzo ya kuimarisha Umma wa Kiislamu.
Jumuiya ya walimu wa hawza ya Qum
Maoni yako